Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu amewataka watendaji wa serikali ambao wanasimamia miradi na fedha za serikali, kuwa wazalendo na kuwajibika ipasavyo kwenye usimamizi wa rasilimali za umma.
Mhe Buswelu ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa mradi wa “RAIA MAKINI”, ambao umefanyika katika ukumbi wa Halmashauri, akiaambatana na KUU Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Lincoln Tamba, Afisa Tarafa wa Kabungu Alison Uisso, Afisa Tarafa wa Mwese Alex John, Kaimu Mkurugenzi wa H/W ya Tanganyika na Afisa Mipango Deus Luziga, Katibu Mtendaji TOSOVC Ndg George Kasabwe, pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya TUPAFO Bwa Alan Kondowe.
“Mradi huu wa RAIA MAKINI, unaenda kutekelezeka huko chini kwenye serikali za vijiji, na unahusu Raia Makini na miongoni mwa watumishi hivyo nimeuzindua mradi huu na niwatake mkafanye yale yanayowahusu na mengine yasiyo kwenye mipango yenu yaacheni kamayalivyo” DC Buswelu
“Lakini pia pamoja na kuzindua mradi huu ila sifurahishwi kwa sababu wanakuja kufanya yale ambayo sisi na ninyi yamewashinda kutekeleza, hii iwe chachu ya ninyi kuwajibika kwenye kazi zenu na kutimiza majukumu yenu kwa uzalendo” Amesema Mhe Onesmo Buswelu.
Aidha kwa upande wa wasimamizi wa mradi huu wa RAIA MAKINI, kutoka Taasisi ya kusaidia watoto yatima na wanaoishi Mazingira hatarishi (TOSOVC) Bw George Kasabwe amesema kwamba mradi huu unatarajia kuelimisha wananchi wapatao milioni tatu (3), kitaifa ambapo kwa Wilaya ya Tanganyika watapita katika vijiji vya Kabanga, Mganza vilevile na maeneo yaliyotajwa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG, ambayo ni Kasekese na Mwese.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya TUPAFO Bw, Alan Kondowe amesema kwamba dhamira ya mradi huu ni kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa fedha za umma, ambapo walengwa wakubwa ni wananchi, hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambao ni walengwa wakuu wa maendeleo.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw Shaban J. Juma, Afisa Mipago Bw Deus Luziga amesema kwamba Halmashauri itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi hizo, hadi kukamilika kwa mradi huo ambao utakuwa wa miezi 18 kwa hapa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.