Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imefanya ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 17 hadi 18 Januari, 2026 kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026.Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi, kutathmini matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali pamoja na kubaini changamoto zinazoweza kuathiri ukamilishaji wa miradi hiyo kwa wakati uliopangwa.
Katika ziara hiyo, Kamati imekagua ujenzi wa Shule ya Msingi Sibwesa unaojumuisha madarasa sita ya elimu ya msingi, madarasa mawili ya elimu ya awali, jengo moja la utawala pamoja na matundu kumi na manne ya vyoo kwa wavulana na wasichana. Kamati pia ilikagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Itunya ambao kwa sasa umefikia hatua ya uwekaji wa dari na upigaji wa ripu.
Vilevile, Kamati imekagua ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Mchangani (Ikola), ambapo mradi huo upo katika hatua ya ufungaji wa renti huku mafundi wakiendelea na kazi za ujenzi.Aidha, Kamati ilitembelea kikundi cha TUJIKOMBOE IKOLA GROUP chenye wanachama watano ambacho kimepokea mkopo wa shilingi 53,000,000 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa ajili ya ujenzi wa ghala (godown) na biashara ya ununuzi na uhifadhi wa mazao, ambapo Kamati ilipongeza juhudi za kikundi hicho katika kuimarisha uchumi wa wananchi.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya walimu aina ya 2:1 katika Shule ya Sekondari Juma Zuberi Homera, ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mchakamchaka, ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Ifukutwa pamoja na ukaguzi wa utengenezaji wa madawati katika Kijiji cha Majalila.Baada ya kukamilisha ziara hiyo, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ilieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, ikibainisha kuwa miradi mingi inaendelea vizuri na inaonesha thamani ya fedha inayotumika.
Hata hivyo, Kamati ilitoa maelekezo na ushauri mbalimbali ikiwemo kuhakikisha mafundi wanalipwa mara moja baada ya kukamilisha kazi walizokabidhiwa bila kucheleweshwa.Kamati pia ilielekeza vikundi vilivyopata mikopo kutoka Halmashauri kufuatiliwa kwa karibu na kuangaliwa namna ya kuviwezesha kupata mtaji wa kununua mazao ili kuimarisha na kuendeleza biashara zao.
Aidha, Kamati ilisisitiza ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mchakamchaka upewe kipaumbele kwa kuongezewa fedha ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. Halmashauri ilishauriwa kutenga fedha mahsusi kwa ajili ya usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha ubora wa kazi na thamani ya fedha inayotumika.Vilevile, Kamati ilitoa maelekezo kwa mafundi na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi kuendelea kupewa elimu juu ya taratibu za uombaji wa zabuni na tenda kupitia mifumo rasmi ya Serikali ikiwemo Mfumo wa NeST, kabla ya kupewa kazi, ili kuongeza uwazi, ushiriki wa wazawa na ufanisi katika utekelezaji wa miradi.Kwa ujumla, ziara hiyo imeendelea kuonesha dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika katika kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo, kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia mipango na bajeti, na kwamba wananchi wananufaika na huduma bora, endelevu na zenye tija kwa maendeleo ya jamii.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.