Katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, viongozi wa wafugaji kutoka Kata 16 wamejumuika pamoja na viongozi wa serikali wa kata, maafisa maendeleo ya kata, wataalam wa ardhi, na maafisa mifugo wa kata zote za Wilaya hii.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kutoa mafunzo kuhusu matumizi bora ya ardhi, ufugaji wa kisasa wenye tija, utunzaji wa mazingira, na mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanganyika, Lincoln Tamba, ambaye amesisitiza umuhimu wa kujitolea na ushirikiano katika kuhakikisha elimu hii inafikishwa kwa wananchi.
Ameeleza kuwa ni muhimu viongozi hawa kuwa na uelewa wa kina kuhusu njia bora za kutumia ardhi na mbinu za kisasa za ufugaji ili kuhakikisha mifugo inapata tija na mazingira yanaendelea kutunzwa kwa manufaa ya jamii.
Katika hotuba yake, Tamba ametoa rai kwa viongozi wa kata na vijiji kuwa wanapaswa kuwa mabalozi wa elimu hii kwa wananchi wao.Amehimiza kusimamia vema shughuli za ufugaji na kuhakikisha kuwa vikao vya kutoa elimu hiyo kwa wananchi vinaandaliwa mara kwa mara, huku taarifa za utekelezaji zikikabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ili kufuatilia mafanikio na changamoto zinazojitokeza.
Mafunzo haya yamelenga pia kuongeza ufanisi katika matumizi ya ardhi, kuhakikisha ufugaji unafanywa kwa njia endelevu, na kutoa mikakati ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zimeanza kuwaathiri wakulima na wafugaji katika wilaya ya Tanganyika.
Wakati wa kikao hicho, wataalam wa ardhi na mifugo wameeleza mbinu mbalimbali za kuboresha matumizi ya ardhi, ikiwemo viwango vya ufugaji wa kisasa na njia za kuongeza tija katika sekta ya mifugo. Vilevile, wamezungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.