Wakulima wa tumbaku Mpanda Kati wasaidia kuezeka vyumba vya madarasa Tanganyika.
Tanganyika. Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Bw. Salehe Mhando amekabidhiwa bandari 18 za mabati yenye urefu wa futi 10 ‘geji’ 28. Mabati hayo yametolewa na chama cha msingi cha wakulima wa tumbaku- Mpanda Kati kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Mkuu wa wilaya ya Tanganyika anayehamasisha wananchi kujitolea kujenga vyumba vya madarasa kwa kila shule.
“Msaada huu umeletwa wakati muafaka, nimeshahamasisha wananchi kujenga wenyewe vyumba vya madarasa na wameitikia kweli kweli.” Amesema Bw.Mhando.
Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ina shule za msingi 52 na wanafunzi wa kuanzia darasa la awali hadi la saba 49,622. Vyumba vya madarasa vipo 320 na upungufu wa vyumba 839. Hadi sasa shule za msingi zina maboma mapya ya vyumba vya madarasa 96 na maboma ya ofisi 20.
Mkuu wa wilaya ametoa wito kwa wadau wa Elimu na wenye mapenzi mema kuendelea kuchangia michango ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa.
Maboma hayo 96 ya vyumba vya madarasa yatakapokamilika, kutabakia na upungufu wa vyumba vya madarasa 743 kwa upande wa shule za msingi kwa sasa. Wakati shule za sekondari zipo 9 tu katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Shule 8 zinamilikiwa na halmashauri ya wilaya ya Mpanda wakati shule moja ni ya watu binafisi.
Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ina kata 16 na kila kata inatakiwa iwe na shule ya sekondari ya kata. Ni kata 8 tu zenye shule za kata na hivyo bado halmashauri inahitaji wadau wa Elimu na wengine kuunga mkono katika kuijenga Tanganyika mpya kielimu, uchumi na kimtazamo kwa ujumla.
Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika amewashukuru bodi ya wakurugenzi wa chama cha msingi cha wakulima wa Mpanda Kati kwa kuwasaidia wananchi wa wilaya ya Tanganyika kwa kuwapa mabati. Hadi sasa yanahitajika mabati 4,512 katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
Naye Meneja wa chama hicho cha wakulima wa tumbaku Mpanda Kati Bw.Rajab Athuman amesema, “chama cha wakulima wa Mpanda Kati kimejikita kurejesha faida kwa wananchi wanaolima tumbaku kwa kusaidia upande wa Elimu kwa kuanzia”. Kwa muda wa miaka mitatu, chama kilijenga nyumba ya mwalimu katika shule ya msingi Mpembe, chumba cha darasa katika shule ya msingi Igalula na tarehe 18/04/2017 kilikabidhi bandari 18 za bati za kuezekea vyumba vya madarasa vilivyopo katika wilaya ya Tanganyika.
Hata hivyo, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Mhe. Hamadi Mapengo amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo ya wilaya ya Tanganyika katika nyanja mbali mbali. Pia aliwashukuru wanachama na wafanyakazi wa chama cha wakulima wa tumbaku wa Mpanda Kati kwa msaada wa mabati ya kuezekea vyumba vya madarasa.
“Binafsi nimefanya kazi katika chama cha Mpanda Kati kwa muda wa miaka 9 nikiwa karani. Najua mchango wao kwa jamii, hasa halmashauri ya wilaya ya Mpanda (Tanganyika)” , amesema Mheshimiwa Mapengo.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.