Wananchi tarafa ya Mwese wapatiwa mafunzo ufugaji nyuki
Zaidi ya wananchi 100 wa vijiji vitano vilivyopo katika tarafa ya Mwese, wamepatiwa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa. Mafunzo hayo yametolewa na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kwa kushirikiana na mradi wa TUUNGANE.
Wananchi hao wa vijiji vya Lugonesi, Mwese, Lwega, Katuma na Kagunga wamefundishwa namna ya kuhuisha katiba za vikundi vyao vya ufugaji nyuki na namna ya kuwa wajasiriamali wa mazao ya nyuki.
Meneja wa uhifadhi mazingira wa mradi wa TUUNGANE, Bw. Peter Lorry amesema kuwa, “TUUNGANE wamekuwa wakishirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda kuandaa na kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vilivyopo wilayani Tanganyika”.
Mradi wa TUUNGANE umenufaisha wananchi wengi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda hasa kwa kuwafundisha wananchi umuhimu wa utunzaji mazingira na namna ya ufugaji nyuki wa kisasa. Hadi sasa, halmashauri ya wilaya ya Mpanda inaongoza kwa kuwa na asali bora. Ubora huo unatokana na kuwa na misitu mizuri inaweza kutoa maua yasiyo ya kemikali na pia elimu ya namna ya kuzingatia usafi wakati wa kuvuna na kuhifadhi asali.
Mradi wa TUUNGANE walitoa msaada wa vifaa vya kisasa vya kuvunia asali kwa vikundi 16 vyenye thamani ya 17 milioni.
Aidha, Bw. Lorry aliahidi kuwagawia mizinga ya kisasa wana vikundi wa vijiji hivyo vitano na kuhakikisha watalaam wanasimamia na kuwaelekeza namna ya kutundika mizinga, kuambika na uelekeo wa jua. Nyuki hawapendi joto kali wala kupigwa na jua. Wanapenda joto la wasitani na sehemu tulivu.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.