Kampuni ya GBP Tanzania imeunga mkono jitahada za Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Mhe. Salehe Mhando kwa kumchangia mifuko 100 ya saruji. Mifuko hiyo imekabidhiwa Aprili 5, 2018 na meneja wa GBP tawi la Katavi Bw. Mark Said.
Bw. Said amesema, “Kampuni ya GBP Tanzania yenye makao Makuu mkoani Mwanza, tumeguswa na uzalendo wa Mkuu wa wilaya ya Tanganyika anayepigania maendeleo ya wakazi wa wilaya yake. Sisi kama wafanya biashara tumeona tuchangie mifuko 100 ya saruji kama sehemu ya kuboresha miundombinu bora ya elimu.”
Mhando ameendelea kuwagusa wadau wengi wa elimu kutokana na utendaji wake wa kazi. Amekuwa akishirikiana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda, kwa maana ya Mkurugenzi mtendaji na watalaam wake pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Mpanda. Mara tu baada ya kufika Tanganyika 2016, Mhando alikuta bkuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na ofisi za walimu.
Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kuwashirikisha wadau mbali mbali wa maendeleo kujitoa kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa miundo mbinu. Wananchi wamemuunga mkono kwa kujenga maboma ya vyumba vya madarasa 135. Sasa ibebakia kazi ya kuenzeka na kuweka malumalu madarasani.
“Bado nahitaji wadau muuendelee kuniunga mkono kwa kuchangia mabati, malumalu na fedha au vifaa vya ujenzi. Tunataka wanafunzi wa Tanganyika wasome kwenye madarasa ya kisasa “ Alisema Mhando.
Naye mwandishi wa habari wa Clouds TV- Katavi, Bw. Ezron Mahanga amefanikiwa kukabidhi mifuko 10 ya saruji kwa Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, ambayo amechangisha kwenye kundi la ‘whatsapp’ lijulikano kwa jina la KISIWA CHA HABARI. Yote haya ni katika kuunga mkono ujenzi wa shule ya sekondari Bulamata (Mishamo).
“Ninawashukuru sana wanakundi walioniunga mkono kunichangia mifuko ya saruji kwa kuungana na wazo langu la kuwiwa kusaidia kuinua elimu wilayani Tanganyika. Nimekuwa naumia sana ninapoenda kufanya kazi zangu za uandishi shuleni ninapoona wanafunzi wamekaa chini au wanasomea nje. Sisi kama wanahabari tuna wajibu wa kukosa, kufichua na kushirikiana na serikali katika kuijenga nchi”. Alisema Mahanga
Hata hivyo Afisa Elimu msingi Bw. Kenny Shilumba ameahidi kuhakikisha kila msaada unaotolewa na wadau wa elimu utatumika kwa malengo kusudiwa.
Wilaya ya Tanganyika ina vijiji 55 lakini shule za msingi zipo 52 zinazotoa huduma ya elimu na tuna sekondari 8 za serikali na 1 ya wawekezaji. Kuna kata 16 na kila kata inatakiwa kuwa na sekondari. Ni kata 8 tuzenye huduma ya elimu ya sekondari. Kata za Kasekese, Sibwesa, Tongwe, Bulamata na Ilangu zimeanza ujenzi wa sekondari na zingine zimefikia katika maboma na zingine kupaua.
Kutokana na kuwepo kwa wanafunzi wapatao 59,126 katika shule za msingi, vyumba vya madarasa vinavyohitajika ni 1437, vilivyopo ni vyumba 314 na hivyo kuwa na upungufu wa vyumba 909 sawa na asilimia 63 hali inayosababisha wanafunzi wengi kusoma chini ya miti. Katika shule za sekondari, mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 120, vilivyopo ni 91na hivyo kuwa na upungufu wa vyumba 29 sawa na asilimia 24.
Katika shule za msingi, madawati yanayohitajika ni 14,373 yaliyopo ni 13,519 na upungufu ni 1031 sawa na asilimia 7.1.Kwa shule za sekondari, mahitaji ya meza/viti ni 4765 na hali ya samani hizo ni 3796 na hivyo kuwa na upungufu wa meza/viti 969 sawa na asilimia 20.3. Mahitaji haya yanazidi kuongezeka kutokana na uandikishaji kuendelea shuleni.
Wananchi wameitikia wito wa ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata ili kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015 na sera ya Elimu ya kuhakikisha kila kata angalau inakuwa na shule moja ya sekondari. Shule zinazojengwa mpaka sasa ni katika kata ya Kasekese ambapo vyumba vitatu vya madarasa na ofisi vinajengwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa ni lenta. Katika kata ya Sibwesa, panajengwa vyumba sita vya madarasa na ofisi moja ya walimu ambapo ujenzi upo hatua ya lenta.
Katika Kata ya Tongwe panajengwa vyumba vitatu vya madarasa na ujenzi upo hatua ya lenta. Kata ya Bulamata wananchi wamejenga vyumba sita vya madarasa. Vyumba vitatu vimepauliwa na vyumba vitatu vinaendelea kupauliwa. Kwa upande wa kata ya Ilangu vyumba vitatu vya madarasa vipo hatua ya msingi. Vile vile katika kata ya Mnyagala, wananchi wametenga eneo la ujenzi wa shule na kazi zinazoendelea ni ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi.
Shule za msingi zinahitaji jumla ya nyumba za walimu 640, zilizopo ni223na upungufu ni417 sawa na asilimia 65.1. Katika shule za sekondari, mahitaji ya nyumba za watumishi ni 170 wakati zilizopo ni 38 na hivyo kuwa na upungufu wa nyumba 132 hali inayoathiri ustawi wa watumishi.
Matundu ya vyoo hutumiwa kwa kuzingatia uwiano wa wanafunzi wa kike 20 kwa tundu moja na wavulana 25 hutumia tundu moja. Katika shule za msingi, pana uhitaji wa
matundu ya vyoo2555 bali yaliyopo nimatundu 497 na hivyo kuwa na upungufu wa matundu ya vyoo 2058 sawa na asilimia 80. Katika shule za sekondari, mahitaji ya matundu ya vyoo ni 173, yaliyopo ni 150 na upungufu ni matunduya vyoo 23 sawa na asilimia 13.
Katika shule za sekondari panahitajika maabara za sayansi 24. Maabara 18 zimekamilika na kuwa na upungufu wa maabara 6 hali inayoathiri ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi sawa na asilimia.
Halmshauri ya Wilaya ya Mpanda inahitaji jumla ya daharia 87 katika shule za sekondari ilhali zilizopo ni 12 na hivyo kuwana upungufu wa daharia 75 sawa na asilimia 86.2. Hali hii husababisha wanafunzi kutembea mwendo mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni na hivyo kupata vishawishi hususani wanafunzi wa kike na hivyo kuathiri maendeleo ya wanafunzi.
Katika shule za msingi, panahitajika maktaba 52. Shule hizi hazina maktaba sawa na asilimia 0. Kwa upande wa shule za sekondarimahitaji ya maktaba ni 08.Maktaba zilizopo ni 2 na hivyo kuwa na upugufu wa maktaba 6 sawa na asilimia 75, jambo ambalo huathiri ari ya wanafunzi kujisomea.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.