Wadau wa Maendeleo Wakutana Kujadili Ustawi wa Mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika
Katika kikao cha kila baada ya miezi 3 kilicholenga kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Awali ya Watoto (PJT-MMMA), wadau mbalimbali kutoka sekta ya elimu, afya na lishe wamekutana kujadili hali ya makuzi, malezi na maendeleo ya watoto ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Changamoto Zilizojadiliwa:
Wajumbe wa kikao wamebainisha changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya mtoto katika eneo la Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika, zikiwemo:
⦁Ukosefu wa vituo vya malezi na maendeleo ya awali ya watoto
⦁Uhaba wa walimu wa shule za awali
⦁Ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya malezi na makuzi ya Watoto.
⦁Bajeti finyu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya watoto
Kwa mujibu wa mjadala, changamoto hizi zimekuwa kikwazo kikubwa katika kufikia malezi bora na maendeleo jumuishi ya watoto katika jamii.
Hatua Zilizopendekezwa:
Mojawapo ya maamuzi makuu yaliyofikiwa ni kuundwa kwa kamati maalum ya kusimamia ujenzi wa vituo vya malezi. Kamati hii itashughulikia:
⦁Kutafuta maeneo sahihi ya ujenzi
⦁Kuandaa bajeti ya utekelezaji
⦁Kusimamia hatua kwa hatua ujenzi wa vituo hivyo
Juu ya changamoto ya ushiriki mdogo wa Wanaume katika makuzi na malezi ya watoto:
Sajenti Cristina kutoka Dawati la Polisi Wilaya ya Tanganyika amesistiza umuhimu wa ushiriki wa wanaume katika malezi ya watoto. Atoa wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya elimu ya malezi, na kwa wanawake kuwahamasisha waume zao kushiriki.
"Rai yetu ni kwamba wanaume mjitokeze tunapotoa elimu katika maeneo yenu. Msiachie wanawake pekee. Ushiriki wa wanaume bado ni changamoto kubwa sana," alisema Sajenti Christina.
Elimu ya Pamoja Kliniki:
Wanawake pia wanahimizwa kuhudhuria kliniki wakiwa na waume zao ili wote wawili wapate elimu ya pamoja kuhusu makuzi na afya ya mtoto. Hii itasaidia kuongeza uelewa na ushiriki wa pamoja katika malezi.
Wito kwa Jamii na Vyombo vya Habari:
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bwana Oscar Mkende, anawaomba wananchi, wadau wa maendeleo, na maafisa habari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kutekeleza mpango huu muhimu wa maendeleo ya awali ya mtoto.
“Kila mmoja wetu asimame kwa nafasi yake kuwezesha malezi bora ya watoto. Bado kuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema.Bwana Oscar,Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.