Wabunge kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma, ambayo inapakana na Ziwa Tanganyika, wameungana katika ziara maalum kutembelea bandari ya Karema, wilayani Tanganyika mkoani Katavi, kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo pamoja na meli nne kubwa zinazojengwa ili kuimarisha usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara katika ukanda huo wa magharibi mwa Tanzania.
Katika ziara hiyo, wabunge hao wameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo kila meli inatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 2,000. Hii imeonekana kuwa hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini, hasa katika Ziwa Tanganyika ambalo lina umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kibiashara kwa Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Zambia.
Wamepongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa kimkakati unaoendelea kufanyika katika sekta ya usafirishaji, hasa kwa kujenga bandari ya kisasa ambayo imeanza kufungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya pembezoni na taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ambaye ameambatana na wabunge hao, ameweka wazi kuwa serikali imejipanga kuifanya bandari ya Karema kuwa kitovu cha biashara, si tu kwa Tanzania bali pia kwa nchi jirani. Ameeleza kuwa uwekezaji unaoendelea una lengo la kuongeza pato la taifa kupitia biashara ya majini.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tanganyika, Mhe. Selemani Kakoso, akizungumza na wananchi wa maeneo ya Karema, ametilia mkazo suala la wakandarasi kuzingatia sheria na taratibu za ajira, hususan kuhakikisha wananchi wa maeneo jirani wananufaika kupitia ajira za muda na za kudumu.
Mradi huu umeonekana kuwa na mchango mkubwa katika kufungua uchumi wa mikoa ya Magharibi na kuiweka Tanzania katika nafasi bora ya kibiashara katika ukanda wa Maziwa Makuu.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.