Timu ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) imebaini kuwa ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, bado ni kijana na haijazeeka kiasi cha kutokidhi mahitaji ya uzalishaji wa mazao ikiwemo zao la Mahindi ambalo ndilo lilikuwa likifanyiwa utafiti.
Wataalamu hao wamefanya tafiti kwenye Vijiji 8, ambapo jumla ya mashamba 389 na wakulima 240 wamefanyiwa utafiti kuhusu aina yao ya ulimaji na utunzaji wa ardhi.
Katika utafiti huo umebainisha kwamba kwa kiasi kikubwa udongo wa maeneo ambayo utafiti huo umefanyika yana upungufu wa rutuba hivyo wameshauri njia za kitalaam kutumika ili kuongeza uzalishaji, maeneo hayo ni kama Ifukutwa, Ngomalusambo, Majalila, Igagala, Mchakamchaka, Kabungu, Kamsanga na Nkungwi.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa niaba ya timu Mhadhili Daniel M. Nhunda amebainisha njia za kufanyika ili kuongeza uzalishaji ni kama; kutumia mbolea kwa awamu tatu kwa kuzingatia muda sahihi, kuacha kuchoma na kupalilia mabaki ya mazao, kutumia chokaa kwa kiasi kikubwa, kufanya tathimini ya udongo ili kubaini mapungufu yaliyopo.
Aidha kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw Shabani J. Juma amesema kwamba kama Halmashauri atahakikisha anarejesha kwa jamii uwezeshaji wa maarifa na ujuzi kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji.
Sambamba na hilo ameiagiza Idara ya Kilimo kuhakikisha ripoti hii iliyowasilishwa wanaibeba na kuifanyia kazi ambapo ametaka wataalamu wafike kwa wakulima na kutoa elimu ya kitalaamu zaidi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.