MKUU WA MKOA KATAVI AZINDUA UPANDAJI MITI-MWESE
Mkuu wa mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga amewaongoza wananchi wa kata ya Mwese katika kuhamasisha upandaji wa miti mkoani Katavi ambapo zaidi ya miti 200 imepandwa katika eneo la kanisa. Zoezi hilo limefanyika Disemea 7, 2017katika kata ya Mwese wilayani Tanganyika .
Wananchi wa Mwese wameitikia kwa wingi na zaidi ya miti 500,000 aina ya misindano (pinus patula) inatarajiwa kugawiwa bure kwa wananchi na taasisi mbali mbali kwa lengo la kupandwa na baadaye ije kuwanufaisha watu mbali mbali. Miti hiyo imefadhiliwa na shirika la kimataifa (THE NATURE CONSERVANCY) kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
Licha ya The Nature Conservancy kufadhili shughuli za uandaaji wa vitalu vya miche ya miti, mradi wa Tuungane umekuwa ukishirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Tume ya Taifa ya mipango ya matumizi bora ya ardhi na wakala wa misitu Tanzania (TFS) katika uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini na usimamizi wa pamoja wa raslimali za misitu katika wilaya ya Tanganyika.
Mojawapo ya faida ya miti hiyo ni pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi kwani mazao ya miti ni biashara. Mbao zinahitajika kwa wingi na kwa kuwa miti hiyo imegundulika kutoa mbao nyingi na nzuri.
Muhuga amesema, “wananchi wa mkoa wa Katavi mnapaswa kuchangamkia fursa zinazojitokeza. Eneo la Mwese kunastawi zao la kahawa, miti na migomba”.
Hata hivyo Muhuga ameongeza kuwa hakuna haja ya kuendelea kutegemea zao la tumbaku kama zao la biashara kwani limekuwa na changamoto ya kuwa na masharti magumu wakati kuna mazao mengine. Mazao mbadala wa tumbaku ni pamoja na kuanzisha mashamba ya miti ya kupandwa, pamba, alizeti, korosho na kahawa.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda mhe. Hamadi Mapengo aliwashukuru wadau wa utunzaji wa mazingira hasa shirika la Tuungane ambao wamekuwa wanashirikiana na Halmashauri katika utunzaji wa mazingira hasa matumizi bora ya ardhi.
Hata hivyo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw. Romuli John amesema, “hata zao la chai linaweza kustawi katika maeneo ya Mwese. Tusiogope kujaribisha kupanda chai kama sehemu ya kujifunza”.
Hali ya hewa ya Mwese inakubaliana na mazao mbali mbali ya biashara bila kusahau matunda. Vyote hivyo vinaweza kukusababishia utajiri uliotukuka na kuwaacha watu wengine wakiwa midomo wazi. Ndizi mbivu zinazopatikana Mpanda mjini, asilimia kubwa zinatoka Mwese.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.