Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu, ametoa maagizo kwa mkandarasi anayesimamia ujenzi wa Daraja la Silonge lililopo katika Kijiji cha Katobo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo tarehe 27 Oktoba, 2025. Lengo ni kuhakikisha daraja hilo linapitika kwa urahisi ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura litakalofanyika tarehe 29 Oktoba.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo chini ya TARURA, Mhe. Buswelu amesisitiza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kwa wakati siyo tu kutarahisisha usafiri bali pia ni sehemu ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki ya kushiriki katika mchakato wa kupiga kura.
Aidha, Mhe. Buswelu amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa uwajibikaji katika zoezi la upigaji kura, akisisitiza kuwa ni haki yao ya msingi na njia ya kuchangia maendeleo ya taifa.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya pia amekagua maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ya Silonge, ambayo imejengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali. Mpaka sasa, zahanati hiyo imegharimu kiasi cha Shilingi milioni 60 na iko katika hatua ya upauaji.
Mhe. Buswelu amepongeza juhudi za wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi huo, na akasisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia kwa karibu.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.