HALMASHAURI YA TANGANYIKA YAWEKA MIKAKATI KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO.
Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi katika kuongeza vyanzo vya mapato inakusudia katika bajeti ijayo kutenga fedha kwa ajili ya kujenga uwanja wa mpira ili kupitia mashindano mbalimbali halmashauri hiyo iweze kujiingizia mapato.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Shaban Juma, wakati akijibu hoja ya Diwani wa Kata ya Tongwe Frank Kibigasi katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani aliyetaka kujua mikakati ya halmashauri katika kubuni chanzo cha mapato kupitia michezo na kusema kuwa tayari ameshampatia maelekezo Afisa Utamaduni kutafuta eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa.
"Katika dunia ya leo sehemu nyingi masuala ya michezo wanayapa umuhimu ila sisi wilayani hapa hatuna kiwanja cha michezo. Tunaangalia eneo zuri ambalo linaweza kuwa kubwa na linafikika na watu kwa ukaribu ili tuweze kuingiza nguvu zetu"
Aidha, Diwani Kibigasi ameishauri halmashauri kuanzisha kituo cha kukusanyia ushuru eneo la Ngomalusambo kwa kuwa eneo hilo mazao yanapitishwa kiholela jambo linaloikosesha halmashauri mapato na kuinufaisha halmashauri nyingine.
Akichangia hoja hiyo, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema kipaumbele cha kwanza cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mapato hivyo halmashauri inapaswa kujipanga kutokana na mahitaji kuongezeka kila leo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Hamad Mapengo amemtaka mkurugenzi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa Baralaza hilo ili kuleta ufanisi katika eneo la ukusanyaji mapato.
Katika hatua nyingine, Mapengo amewaomba Madiwani kuisaidia Serikali kuhimiza watoto waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza kuripoti haraka Shuleni.
"Turudi kwenye Kata zetu tuwahimize watendaji wa Vijiji. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi sana za kukamilisha miundombinu ya ujenzi wa madarasa,nyumba za walimu, tumepata fedha za madawati mmeona na Watumishi wanaendelea kufika kwa hiyo kazi yetu ni kuhakikisha tunahimiza wale watoto waende wakaripoti"
Katika shule ya Sekondari Majalila wanafunzi wapatao 27 bado hawajaripoti hadi sasa licha ya masomo kuanza jambo ambalo Mkuu wa wilaya ameagiza wanafunzi hao wabainishwe na wasakwe ili wakajiunge na masomo.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.