Tanganyika DC, Katavi – Oktoba 2, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, amefanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa meli nne za mizigo. Katika ziara hiyo, Mhe. Mrindoko ametoa maagizo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kuhakikisha maeneo ya kimkakati, ikiwemo Karema, yanapimwa na kurasimishwa kwa lengo la kuongeza thamani ya ardhi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Akiwa katika bandari hiyo ambayo tayari imeanza kutoa huduma mbalimbali, RC Mrindoko ameeleza kuwa kukamilika kwa meli hizo kutafungua fursa nyingi kwa wakulima na wafanyabiashara wa Mkoa wa Katavi na maeneo ya jirani kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na mazao kuelekea masoko ya kitaifa na kimataifa.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Katavi. Ni wakati sasa wa kuzalisha mazao ya kutosha kwa ajili ya masoko ya ndani na nje, kwa kuwa Bandari hii itakuwa lango la kibiashara litakalotuunganisha na masoko makubwa zaidi,” amesema RC Mrindoko.
Pia Katika kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha wananchi moja kwa moja, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bw. Shabani Juma Juma, kuhakikisha upimaji na urasimishaji wa maeneo unatekelezwa kwa kasi.
“Namuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kuendeleza upimwaji wa ardhi katika maeneo haya na urasmishwaji wa maeneo haya ili kuyaongezea thamani, tusiachwe nyuma tuchangamkie fursa hizo.” RC Mrindoko.
Licha ya agizo hilo la Mkuu wa Mkoa wa Katavi, tayari Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imekwisha aanza urasmishaji wa maeneo ya kimkakati ambapo timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imeanza zoezi hilo kwa kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Kasekese ambayo ni eneo moja wapo miongoni mwa maeneo yenye mzunguko mkubwa wa biashara na idadi kubwa ya makazi ya wananchi.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Bandari ya Karema, Bw. Antony Poyo, anaeleza kuwa ujenzi wa meli hizo umefungua fursa za ajira kwa wakazi wa eneo hilo kupitia kazi za muda na ushiriki wa jamii katika huduma mbalimbali zinazohusiana na mradi.
Serikali kupitia taasisi husika inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuiunganisha Bandari ya Karema na maeneo mengine muhimu, ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mpanda hadi Karema pamoja na mpango wa kuunganisha bandari hiyo na reli ya kisasa ya SGR. Hatua hizi zote kwa pamoja zinatarajiwa kuifanya Bandari ya Karema kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara na maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.