MKURUGENZI TANGANYIKA ATANGAZA KUANZA HAMASA ZA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, WANANCHI WAITWA KUJIANDIKISHA KWA WINGI, WENYE SIFA ZA KUGOMBEA UWANJA NI WAO.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw. Shaban J. Juma leo ametangaza rasmi kuanza kwa Hamasa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kote nchini,
Akitoa Tangazo hilo, Bw. Shaban Juma ameweka bayana mtiririko wa matukio mbalimbali ambayo yatafanyika mpaka kuifikia siku rasmi ya kuchagua viongozi wa serikali za vijiji, mitaa na vitongoji,
Pia Bw. Shaban Juma aliongeza kwa kuwataka wananchi wote wilayani Tanganyika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ifikapo tarehe 11-20.10.2024 sambamba na wenye sifa za kugombea wasisite wajitokeze waweze kugombea,
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Alphonce Mwakyusa aliwataka wahusika wote wa uchaguzi wa serikali kuhakikisha wanazingatia kanuni na taratibu za uchaguzi huo ili kuepusha migongano isiyokuwa ya lazima,
Vilevile, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi wilayani Tanganyika Bw. Issa Bida alisema kuwa wamepokea kwa mikono miwili tangazo hilo na sasa ni wajibu wao kuwambusha wananchi na wanachama wao kujiandaa na uchaguzi huo ikiwemo kujiandikisha na wenye sifa za kugombea basi wagombee,
Aidha, Katibu wa Chadema wilaya ya Tanganyika Bw. Thomas Masanja alitoa rai kwa Msimamizi wa Uchaguzi kwa wilaya ya Tanganyika kuhakikisha wanavishirikisha vyama vyote kwa hatua zote ili kuweza kufanikisha zoezi hilo kwa pamoja,
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 utafanyika siku ya tarehe 27.11.2024 na kwa wilaya ya Tanganyika, Jumla ya Tarafa 3, Kata 12, Vijiji 39 na Vitongoji 190 vitashiriki.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.