Katika maandalizi ya msimu mpya wa kilimo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Mhe. Samson Poneja, amefika Kata ya Kasekese, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kutoa mafunzo na kuhamasisha matumizi ya mbolea, pembejeo na mbegu bora kwa wakulima.
Akimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Poneja amewaomba wakulima wa eneo hilo kujizatiti kufuata taratibu zote za kilimo, kuanzia maandalizi ya mashamba, kupanda hadi kuvuna ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mheshimiwa Poneja pia amesisitiza umuhimu wa wakulima kutambua hali ya udongo wa mashamba yao. Amesema serikali imesambaza mashine za kupima ubora wa udongo ili wakulima waweze kujua rutuba ya ardhi yao na kupata ushauri wa kitaalamu juu ya pembejeo zinazofaa.
“Tunaposema ‘mali shambani silaha mbolea’, ni lazima tuhakikishe afya ya udongo katika maeneo yetu ni nzuri, ndomana serikali imesambaza mashine kwajili ya kupima afya ya udongo na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya virutubisho na pembejeo sahihi za kuweka kwenye eneo lako.,” amesema Mhe. Poneja.
Aidha, amewaagiza wakulima kujisajili kwenye daftari la wakulima kupata namba ya mkulima, hii ni hatua muhimu ambayo itawawezesha kunufaika na mpango wa ruzuku wa serikali kwa pembejeo na mbolea.
Zoezi hilo la mafunzo limeambatana na utekelezaji wa uandikishaji wa wakulima na ugawaji wa namba kwa wale waliokuwa tayari wamejiandikisha kwenye daftari la mkulima.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.