MKURUGENZI HALMASHAURI WILAYA YA MPANDA AONGEZA MILANGO YA MAWASILIANO KWA WATUMISHI.
Watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda wameagizwa kutoa taarifa ofisi ya Mkurugenzi mtendaji na kitengo cha habari za miradi na usimamizi wa shughuli zinazoendelea katika maeneo ya kiutendaji.
Maagizo hayo yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw. Romuli John Aprili 27, 2017 alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa viongozi wa kata na kukagua miradi inayoendelea. Bw. John ameanza na kata za Katuma na Mwese ambapo aliongea na viongozi wa Kata na vijiji. “Lengo la ziara hii ni kutaka tufahamiane, kuelekezana na kusikiliza kero na ushauri….”. Alisema Mkurugenzi John.
Ziara ya kutembelea kata zingine 14 zilizobakia katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda atapanga ratiba kuendana na upatikanaji wa muda. Jiografia ya maeneo ya wilaya ya Mpanda huwezi kufanya mikutano kwa zaidi ya kata mbili kwa siku. Mara baada ya kuteuliwa, alikutana na maandalizi ya kukimbiza mwenge kwa halmashauri ya wilaya ya Mpanda. Mwenge ulikimbizwa Aprili 3, 2017 na kuzindua miradi mbali mbali na mingine kuiwekea jiwe la msingi.
Hata hivyo Mkurugenzi John amesema kuwa amekuwa anapata taabu sana kuidhinisha malipo ya ujenzi wa miradi ambayo haijui imefikia hatua gani. Kuanzia sasa anahitaji taarifa ya kila kitu kinachoendelea na siyo kuwa mgeni wa kila jambo au mradi. Wananchi ambao tunawategemea kushirikiana katika shughuli za maendeleo wamekuwa wakilalamikia mkanganyiko wa taarifa.
Lakini pia kuna maelekezo yanayotolewa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Wilaya au Mwenyekiti wa halmashauri au Mkurugenzi kwenda kwa uongozi wa kata au kijiji na maagizo hayo yanakuwa yametolewa zaidi ya wiki 2 au 3 kwa wakuu wa Idara au Vitengo ili wayashushe kwa watendaji wa chini. Sasa kiongozi akienda kukagua utekelezaji wa maagizo anakutana na mshangao kutoka kwa viongozi wa kata au vijiji kwa kutokuwa na taarifa ya maagizo hayo.
Kila mtumishi wa halmashauri ameajiliwa na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji. Sasa itakuwa ajabu katika maeneo yako ya kiutawala ukutane na watu wanaoiba au kutorosha mali au mapato ya halmashauri ushindwe kutoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa kuhofia kuwa unaingilia majukumu ya watu wengine. Mawasilia ya uzalendo, ulinzi au kuzuia uovu hayahitaji kufuata mnyororo wa mawasiliano ya kiutumishi, kama una uhakika na ushahidi wasiliana na Mkurugenzi kwa namba ya simu ya mkononi.
Viongozi wetu wamekuwa na utaratibu wa kugawa namba za simu kwa wananchi ili kuondoa urasmu wa kuwapatia huduma wananchi. Watumishi wa serikali wameajiriwa kwa lengo la kuwahudumia wananchi na pale wananchi wanapoona hawatendewi haki au kupatiwa huduma ya ofisini, wana haki ya kumjulisha Mkurugenzi Mtendaji au hata Mkuu wa wilaya.
Serikali ya awamu ya tano (5) chini ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli imejipanga kuwahudumia wananchi kwa kiwango cha juu. Shida iliyokuwepo kulikuwa hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya watumishi wa umma na wananchi. Pia kulikuwa na mkanyiko wa utoaji wa taarifa kutoka juu kwenda chini au chini kwenda juu.
Uongozi wa kata ya Mwese walimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Bw. John kwa kuandaa ziara ya kuwatembelea viongozi hao. Waliongeza kwa kusema kuwa wamezoea kuwaona wakurugenzi kwenye ziara za kuambatana na Mkuu wa wilaya au Mkuu wa mkoa.
Bw. Romuli John aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda Disemba 19, 2016 baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Bw. Ngalinda Hawamu kufariki Dunia Disemba 1, 2016. Marehemu Ngalinda aliteuliwa Juli 12, 2016 na kudumu kazini kwa cheo cha Ukurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpanda kwa muda wa miezi 5.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.