Wananchi wilayani Tanganyika wametakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili waendelee kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mheshimiwa Jackson G. Kiswaga wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Mheshimiwa Kiswaga amesema kuwa, Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akishusha fedha nyingi maeneo mengi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo ni wajibu wao wananchi kumuunga mkono kiongozi wao huyo.
“Wananchi wa Kijiji hiki cha Kapanga na Tanganyika kwa ujumla endeleeni kumuunga mkono Rais wetu ili na yeye aendelee kupambana kutafuta fedha kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo kama hii” amesema Mhe. Kiswaga,
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imetembelea na kukagua miradi mitatu ya urejeshwaji katika kijiji cha Kapanga ambayo ni Shamba la Malisho ya Mifugo, Banio, Josho na Birika la Kunyweshea mifugo ambayo kwa ujumla wake imegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 80.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Onesmo Buswelu (Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika) ameipongeza Kamati hiyo na kuitaka kufikisha salamu za wananchi wa Tanganyika kwa Rais Samia na na kumshukuru kwa kupeleka zaidi ya shilingi trilioni 1 za maendeleo katika mkoa wa Katavi.
Aidha, baadhi ya wafugaji wa Ng’ombe katika kijiji cha Kapanga wakiwakilishwa na Bw. Joseph Lyataa wameishukuru serikali kwa miradi hiyo huku wakiiomba kuendelea kuwakumbuka kwa miradi mingine ya maendeleo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Miradi ya urejeshwaji wa mazingira nchini inaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania na katika wilaya ya Tanganyika imefanikiwa kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya ufugaji, kilimo na ujasiriamali.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.