Majalila Tanganyika.
Wananchi wa Kijiji cha Majalila Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wameungana na Serikali kujenga kituo cha Polisi kwa kuchangia fedha na nguvu kazi.
Akitoa shukrani kwa wananchi na wadau mbalimbali waliochangia ujenzi wa kituo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu wakati akipokea mifuko 50 ya Saruji yenye thamani ya Tsh. Milioni Moja kutoka kwa Mbunge wa Jimbo Mpanda Vijijini Seleman Kakoso,Buswelu amemuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kuhakikisha wanasimamia michango hiyo kusiwepo upotevu wa aina yoyote.
"Serikali ya Wilaya pamoja na wananchi wote na nguvu ya Mhe. Mbunge Kakoso wameamua kushirikiana kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga kituo cha Polisi cha kisasa,nawashukuru sana"
Akikabidhi mifuko hiyo kwa niaba ya Mbunge, Katibu wa Mbunge Said Wambali amesema ofisi ya mbunge imeona iungane na wananchi pamoja na wadau kuunga juhudi za Serikali kujenga kituo hicho ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kituo hicho,Ramadhan Nyembe amemhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa michango iliyotolewa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali haitapotea na atahakikisha inasimamiwa kikamilifu.
Jofley Makamba mkazi wa Kijiji cha Majalila amesema kukamilika kwa kituo hicho kutawasaidia kuishi kwa amani kwa kuwa wanaamini uhalifu utadhibitiwa na itawarahisishia kufikika kwa haraka kituoni hapo kwani kwa sasa wanafuata huduma Kibo ambapo ni umbali wa kilomita takriban 10 kutoka Kijijini hapo.
Hadi sasa ujenzi upo hatua ya msingi ambao umechimbwa kwa nguvu za Wananchi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.