Mkuu wa mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga amewatahadharisha wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda (Tanganyika) kutoendesha wala kujihusisha na shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo yaliyotengwa kama ushoroba, misitu ya kijiji au maeneo tengefu. Tahadhari hiyo ameitoa kwenye mkutano wa hadhara katika kata za Isengule na Ikola Agosti 4, 2017 wakati alipofanya ziara ya kikazi.
Akijibu swali la mwananchi wa Isengule Bw. Magele Kisoyi aliyetaka kufafanuliwa kama Mijeti ni hifadhi au sehemu ya kuishi binadamu, Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliwajibu wananchi kuwa hawatakiwi kurudi kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo hayo kwani eneo la Mijeti lilitengwa kama msitu wa kijiji na mapito ya wanyama pori kutoka Katavi na Kigoma.
“Wakoloni hawakuwa wajinga kutenga ushoroba wa wanyama miaka ya 1950 na ninawaagiza Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi, atakayethubutu kulima kwenye ushoroba au maeneo tengefu mazao yake yote yafyekwe na kuchukuliwa hatua za kisheria”. Alisema Muhuga.
Kijiji cha Isengule kilifanyiwa matumizi bora ya ardhi na bado kina akiba ya ardhi ya kilimo hadi miaka 50 ijayo. Muhuga aliwashangaa wananchi wa Isengule wanaolalamika kuwa hawana maeneo ya kulima wakati eneo lililotengwa kwa shughuli za kilimo bado kubwa sana na hajui kwa nini wanakimbilia Mijeti ambapo ni mbali sana kutokea katika kijiji cha Isengule. Kutoka Isengule hadi Mijeti ni zaidi ya Kilomita 25.
Matumizi bora ya ardhi yanafanywa na uongozi wa kijiji na hupanga matumizi ya ardhi kulingana na idadi ya wananchi wake katika kijiji husika, idadi ya mifugo, huduma za kijamii na kuangalia zaidi ongezeko la watu katika kijiji kwa miaka 50 ijayo. Kila kijiji kina mipaka yake, uongozi na mamlaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za halmashauri za vijiji.
Shida kubwa ipo kwa viongozi wa vitongoji, vijiji na watendaji wa vijiji ambao huwapokea wahamiaji haramu pasipo kufuata utaratibu wa kijiji husika. Mtu yeyote anayetaka kuhamia katika kijiji sharti aandike barua kwa uongozi wa kijiji kuomba kuhamia katika kijiji husika na akieleza shughuli anayotaka kufanya katika kijiji hicho, idadi ya mifugo aliyonayo na ukubwa wa familia yake. Baada ya barua hiyo uongozi wa kijiji utaitisha mkutano wa hadhara kujadili maombi ya watu wanaotaka kuhamia katika kijiji hicho.
Hata hivyo, Mkuu wa mkoa aliwaagiza watendaji wa vijiji kuwa na madaftari ya wenyeji wa kijiji husika na wageni. Madaftari hayo yaandikwe watu wote yaani nyumba kwa nyumba na namba zao za simu. Na mgeni lazima aandikwe kwenye daftari la wageni akionesha ametoka wapi, anaenda wapi na hapo kijijini atakaa kwa muda gani na akifanya shughuli gani na nani mwenyeji wake.
Kiongozi wa kijiji atakayekiuka utaratibu huo atachukuliwa hatua kwani ataonekana kama yeye ndiye mchochezi wa migogoro kati ya wenyeji na wageni. Utafiti unaonesha kuwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji inasababishwa na wahamiaji haramu. Kuna watu wachache wanaowatapeli wafugaji au wakulima kuwa wao ndio wamiliki wa maeneo ya kilimo au mapori ya misitu hata mabonde ya mito na hivyo kuwaomba wawauzie maeneo hayo. Sasa wale wageni huamini kuwa wanaishi kihalali kwenye maeneo hayo waliyotapeliwa na wahuni wachache.
Kama wewe ni mgeni na unahitaji eneo la kuchungia mifugo au kuendeshea shughuli za kilimo, ni vema ukafika kwenye ofisi za kijiji husika au ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda (Tanganyika) ili kupatiwa huduma unayohitaji.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.