Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu na Milima ya Ntakata (JUMIMINTA) imetakiwa kuendelea kusimamia vyema zoezi la uhifadhi wa misitu ili iweze kuendelea kuleta tija kwa wananchi wanaozungukwa na misitu hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw. Clavery Reginald Vallence alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika katika kikao kilichofanyika jana na leo kilichohusisha Jumiminta na wadau wa maendeleo na uhifadhi wa misitu wilayani Tanganyika.
Bw. Clavery amesema kuwa, misitu imekuwa na mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya wilaya ya Tanganyika na vijiji vyake hivyo ni ni lazima misitu hiyo ilindwe na kuhifadhiwa kwa wivu mkubwa,
“Sote ni mashahidi, wilaya yetu imekuwa ikinufaika kwa kiwango kikubwa kutokana na biashara inayohusisha uhifadhi wa misitu, biashara ya Kaboni, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha misitu yetu inalindwa kwa wivu mkubwa” amesema Bw. Clavery.
Katika hatua nyingine, Bw. Clavery amewataka wasimamizi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika vijiji vyote nane vinavyonufaika na biashara ya Kaboni kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na haraka ili iweze kunufaisha wananchi wa maeneo husika,
Aidha, viongozi wa serikali za vijiji vinavyonufaika na biashara ya Kaboni katika wilaya ya Tanganyika wamekumbushwa kufanya mikutano ya kijiji katika kila robo ya mwaka ili kuweza kufanya tathimini mbalimbali za uhifadhi wa misitu, maendeleo ya miradi na mapato na matumizi ili kuweza kuleta dhana ya uwazi na uwajibikaji katika maeneo yao.
Wilaya ya Tanganyika imejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kwa kufanikiwa kutekeleza vyema biashara ya Kaboni na kuwezesha kuiingizia halmashauri ya wilaya hiyo mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 22 tangu kuanza kwa biashara hiyo mpaka sasa
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.