DC ONESMO BUSWELU AKABIDHI MIFUKO YA SARUJI KUCHOCHEA UJENZI WA BWENI JIPYA LA WASICHANA SIBWESA SEKONDARI.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu, amekabidhi mifuko ya saruji sita (6) kwa Shule ya Sekondari Sibwesa katika kuchochea ujenzi wa bweni la wasichana katika shule hiyo, bweni linalogharimu kiasi cha shilingi milioni 28.Hii ni katika kumwakilisha mdau wa maendeleo ya elimu, Bw. Peter Chilangazi kutoka Dodoma, ambaye ameguswa na juhudi za wananchi wa Kijiji cha Sibwesa waliochangia kiasi cha shilingi milioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo jipya la wasichana katika Shule ya Sekondari Sibwesa.
Mdau huyo amevutiwa na juhudi za wananchi walizoonesha katika ujenzi wa mradi wa Shule Mpya ya Msingi Sibwesa, uliopo kwenye eneo la Shule ya Sekondari Sibwesa. Mradi huo unagharamiwa na fedha za Serikali Kuu (BOOST) kwa gharama za shilingi milioni 342. Mradi huo unategemewa kukamilika mwezi wa 12 mwaka huu na kuanza kazi rasmi Januari mwaka 2026.
Katika kuchochea hilo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu, amemuagiza Mtendaji wa Kijiji kutangaza kwa haraka sana tenda ya ujenzi wa bweni hilo la wasichana ili ujenzi uweze kuanza mara moja kwa manufaa ya wanafunzi wa kike waliopo shuleni hapo.
“Ukitoka hapa, nenda ukae kwenye mfumo. Kesha mpaka asubuhi uwe umeshatangaza tenda hiyo, sababu tumesha chelewa, na wanafunzi wa Sibwesa wanatakiwa kuanza kulala kwenye bweni jipya. Kwa sasa wanatumia darasa kama mbadala wa bweni. Hakuna kisingizio cha kucheleweshwa kwa kutangazwa kwa tenda hiyo,” amesema Mhe. Buswelu.
Sambamba na ziara hiyo ya kukabidhi mifuko ya saruji, Mheshimiwa DC Buswelu amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa shule mpya ya msingi Sibwesa, ujenzi unaohusisha majengo ya utawala, madarasa ya shule ya msingi na awali. Amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi huo kwani unatakiwa kukamilika kwa wakati, mwezi wa kumi na mbili, ili uweze kutumika mwakani bila kuwepo kwa changamoto yoyote kwa wanafunzi.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.