Wananchi wilayani Tanganyika wameshauriwa kuacha kulima kwa mazoea na badala yake waanze kulima kisasa ili waweze kupata mavuno mengi zaidi,
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Onesmo Buswelu alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za kilimo kwa wakulima wa Pamba na Mahindi katika kijiji cha Kagunga kilichopo katika kata ya Kasekese wilayani humo.
Mheshimiwa Buswelu amewataka viongozi wa AMCOS na Maafisa Ugani kuwasaidia wakulima waweze kufanya shughuli za kilimo chenye tija ili waweze kunufaika vya kutosha,
“Viongozi wa AMCOS na Maafisa Ugani shirikianeni na wakulima hawa ili waweze kuanza kuzalisha mazao yao kitaalam na waweze kupata mavuno ya kutosha ili uchumi wao uweze kuinuka” amesema DC Buswelu,
Aidha, Mheshimiwa Buswelu ameendelea kuwakumbusha wananchi wa maeneo hayo kuacha kulima kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kama Misitu, Hifadhi na Ushoroba kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria na serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kufanya hivyo,
Mwisho Mheshimiwa Buswelu amewakumbusha wazazi wote kuhakikisha wanaandikisha watoto wao wadogo na shule na wale ambao tayari wako mashuleni basi wahakikishe wanawapeleka shuleni mara moja shule zitakapofunguliwa Januari 13, 2025.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.