Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mheshimiwa Onesmo Buswelu ameuagiza uongozi wa kata ya Sibwesa wilayani humo kuhakikisha mpaka kufikia kesho wanafunzi wote zaidi ya 130 ambao walikuwa hawajaripoti shuleni wawe wameripoti shuleni,
Agizo hilo limetolewa leo wakati wa ziara ya kukagua hali ya wanafunzi kuripoti shuleni na kuhamasisha suala zima la lishe ili kuondokana na udumavu katika wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi kwa ujumla,
Mheshimiwa Buswelu ameongeza kwa kuwataka wote wanaohusika na masuala ya elimu katika wilaya ya Tanganyika kuhakikisha wanaunda mpango mkakati utakaowawezesha wanafunzi wote ambao hawapo mashuleni wawe wameripoti shuleni kuendelea na masomo kama kawaida,
“Nakuagiza Afisa Tarafa shirikiana na Watendaji Kata na Vijiji na Serikali zote za Vijiji kuhakikisha wanafunzi hawa zaidi ya 130 mpaka kufikia siku ya kesho wawe tayari wameripoti kwenye shule zao” amesema DC Buswelu,
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Buswelu ameutaka uongozi wa shule ya sekondari ya Sibwesa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kupata chakula shuleni hapo chakula ambacho kina mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ili wanafunzi wasipatwe na tatizo la udumavu ambapo katika kusaidia hilo, Mheshimiwa Mkuu wa wilaya ameshiriki zoezi la kupanda miti ya matunda aina ya mapera 20 na kutaka miti hiyo itunzwe ili wanafunzi wapate matunda shuleni hapo,
Vilevile, Mheshimiwa Buswelu ameahidi kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kuwatafutia Ng’ombe wa Maziwa ili wanafunzi hao waanze kupata uji wenye mchanganyiko na maziwa kuboresha afya zao,
Aidha, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Sibwesa Bi. Ernesta Chapuga amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika kwa kutenga muda wa kutembelea shuleni ambapo amemuahidi miti yote iliyopandwa leo itatunzwa ili iweze kuleta manufaa kwa wanafunzi waliopo na wale watakaokuja hapo baadae,
Mkoa wa Katavi licha ya kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao ya chakula, bado hali ya udumavu kwa watoto iko kwa kiwango kikubwa hali iliyopelekea mkoa huo kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha unaondokana na tatizo hilo.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.