Wananchi na Wafanya biashara wasafirishaji wa bidhaa katika Mwambao wa ziwa Tanganyika wametakiwa kuachana na Bandari zisizo rasmi na badala yake kutumia Fursa ya Bandari ya kisasa ya Karema iliyoanza kutumika 1 Septemba 2022 kwa shughuli za kusafiri na Usafirishaji wa Bidhaa zao.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe.Onesmo Buswelu amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Mrindoko ambapo 1 Septemba 2022 amefika katika Bandari ya Karema kushuhudia kuanza kwa shughuli za usafirishaji Bandarini hapo.
Akizungumza na Baadhi ya Wananchi Bandarini hapo DC Buswelu amewataka Wananchi na Wafanyabiashara wanaofanya shughuli za Usafirishaji katika mwambao wa Ziwa Tanganyika pamoja na Wananchi watakaosafiri kupitia Bandari mpya kutunza Miundombinu ya Bandari hiyo kusudi iweze kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
Mhe.Buswelu ameitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA pamoja na Shirika la Uwakala wa Meli Nchini TASAC kushawishi Meli kubwa kutoka Kongo na Maeneo mengine kutia nanga katika Bandari ya Karema.
Shabani Juma, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganganyika amemshukuru Rais Samia kwa Ujenzi wa Bandari hiyo ambapo ametoa rai kwa Wafanyabiashara wanaosafiri kwenda Kongo kutoka Dar es slaam na Maeneo mengine Nchini kutumia Barabara ya Tabora Mpanda iliyo katika kiwango cha Lami kurahisisha kufika kwa urahisi katika Badari ya Karema.
Naye Diwani wa Kata ya Karema Bw. Michael Kapata pamoja na shukrani alizozitoa kwa Serikali amesisitiza juu ya umuhimu wa Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami kutoka Mpanda Karema ili kurahisisha shughuli za Uchukuzi na Usafirishaji wa Bidhaa kutoka Mpanda Mjini hadi Karema Bandarini.
Kaimu Meneja Mfawidhi wa bandari za TPA Ziwa Tanganyika Edward Mabula ameeleza kuwa Zaidi ya boti 4 za Abiria pamoja na Boti za Utalii zimewasili Bandarini hapo ambapo abiria 35 wamepokelewa katika Bandari hiyo wakitokea maeneo mbalimbali ya mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Bandari hiyo iliyogharimu Bilioni 47.9 ilihusisha ujenzi wa kivunja mawimbi, mlango bandari na gati ya meta 150 zenye uwezo wa kulaza meli zenye urefu wa meta 75 na upana wa meta 15, uchimbaji na uwekaji wa kina wa mlango wa bandari, jengo la ofisi, sebule ya abiria na shehena ya jumla.
TONGWE - MAJALILA
Sanduku la barua: S.L.P 01 KATAVI - TANGANYIKA
Telephone: +255-252955264
Simu ya mkononi: 0754870344
Barua pepe: ded@tanganyikadc.go.tz
Copyright ©2018 Tanganyika-DC . All rights reserved.